Mfungwa kijana wa Ujerumani aliyebadilishwa na muuaji wa Urusi

 

Mfungwa kijana wa Ujerumani aliyebadilishwa na muuaji wa Urusi

x

CHANZO CHA PICHA,LIK FAMILY

Maelezo ya picha,Kevin Lik alipelekwa katika hospitali ya Ujerumani kwa uchunguzi baada ya kuachiliwa
  • Author,Sergei Goryashko
  • Nafasi,BBC

Kevin Lik (19) pamoja na mwandishi wa habari wa Marekani Evan Gershkovich, ni miongoni mwa watu 16 walioachiliwa na Urusi tarehe 1 Agosti, katika mpango wa kubadilishana wafungwa kati ya Marekani na nchi nyingine za Magharibi.

Kijana huyo - mwenye uraia wa Urusi na Ujerumani - alikamatwa mwaka jana akiwa bado shuleni na akawa mtu mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya Urusi ya sasa kuhukumiwa kwa uhaini.

Kevin alizaliwa mwaka 2005 huko Montabaur, mji mdogo magharibi mwa Ujerumani. Mama yake Mrusi, Victoria, aliolewa na raia wa Ujerumani, ingawa ndoa haikudumu, yeye na mwanawe walibaki Ujerumani.

Walitembelea Urusi kila baada ya miaka kadhaa hadi Victoria alipoamua kurudi moja kwa moja. Kevin alikuwa na umri wa miaka 12 walipohamia huko 2017.

Waliishi nje kidogo ya mji wa North Caucasus, katika ghorofa yenye kutazamana na milima na kambi ya kijeshi. Kevin anasema alipenda kusoma shuleni na nje ya shule kutembea mashambani na kukusanya mimea kwa ajili ya uwanja wake wa mitishamba.

Ananionyesha vyeti vya mashindano ya kitaaluma ambayo alishinda.


Kuibadilisha picha ya Putin

XC

CHANZO CHA PICHA,ADYGHE STATE UNIVERSITY

Maelezo ya picha,Kevin (wa pili kutoka kulia) alikuwa katika kikundi cha wanafunzi bora waliokutana na Naibu Waziri Mkuu Dmitry Chernyshenko (kushoto) mwaka 2022.

“Ilikuwa ni uchaguzi wa rais wa Urusi wa 2018 ndipo shauku yake na siasa ilipoibuka,” anasema Mama yake - mfanyakazi wa afya katika sekta ya umma.

Kevin alikasirika kwamba karibu kila darasa katika shule yake lilikuwa na picha ya Putin. "Lakini walituambia mara kwa mara kuwa shule sio mahali pa siasa," anasema.

Mwaka mmoja au zaidi, alifanya tukio kubwa pale alibapoidilisha picha ya shule ya Putin na kiongozi wa upinzani Alexei Navalny.

"Mwalimu mmoja alisema wakati wa Stalin, ningepigwa risasi," anasema Kevin - na mwalimu mwingine mwenye huruma, alimshauri kuwa mwangalifu.

Mama yake aliitwa shuleni: "Walimkaripia, wakamfokea," anasema.

BBC imeomba shule kutoa maoni, lakini haijapata jibu.

Kevin alipokaribia mwaka wake wa mwisho wa shule, mama yake aliamua warejee Ujerumani. Wakati huo Urusi ilikuwa tayari imeivamia Ukraine, na ili kuondoka Urusi, jina la Kevin inabidi liondolewe kwenye rejista ya kijeshi.

Victoria alialikwa kwenye ofisi ya uandikishaji kuhusu karatasi za mtoto wake. Alipofika tarehe 9 Februari 2023, polisi walimshutumu bila ushahidi kwamba ametoa matusi hadharani. Alihukumiwa kifungo cha siku 10, hilo lilimaanisha mpango wao wa kuondoa utachelewa.

Kesi ya Jinai

DFXC

CHANZO CHA PICHA,FSB

Maelezo ya picha,Maafisa wa FSB walirekodi upekuzi wao kwenye nyumba ya Kevin na kuiweka video hiyo mtandaoni - mamake Kevin amesimama karibu naye

Victoria alipoachiliwa, walijaribu kwenda Ujerumani kwa kupitia kusini kwenye jiji la Sochi, ambalo lina uwanja wa ndege wa kimataifa.

Baada ya kuingia hotelini, Kevin anasema walitoka kutafuta vitafunio na akagundua mwanaume aliyevalia barakoa na kofia akiwarekodi kwenye simu yake. Anasema, ndani ya sekunde chache, basi dogo lilisimama mbele yao.

"Maafisa wanane au tisa wa shirika la kijasusi la FSB walitoka kwenye gari. Mmoja alinishika mkono. Mwingine akaja, akaonyesha kitambulisho chake, na kusema: 'Kesi ya jinai imefunguliwa dhidi yako chini ya kifungu cha 275: uhaini.'

"Macho yangu yalifunguka kwa mshtuko."

Gari hiyo iliwapeleka hotelini, ambapo walikusanya mizigo yao. Wakiwa njiani kurudishwa Maykop waliwekwa kwenye gari lisilo na namba za usajili na kupelekwa kwenye mkahawa wa piza.

“Waliagiza piza na kutupa. Hawakunifunga pingu wala kunizuia. Nilikuwa nikifikiria kila kitu kichwani mwangu lakini sikuelewa uhai nilioufanya,” anasema Kevin.

Walifika nyumbani katikati ya usiku. Ananionyesha video ya maafisa wa FSB wakipekua nyumba yao. Walipata darubini iliyovunjika - zawadi ya zamani ya kuzaliwa kutoka kwa mama yake.

Mamlaka zilishuku kuwa alikuwa ameitumia kupiga picha magari ya kijeshi kutoka katika dirisha lake na kutuma kwa ujasusi wa Ujerumani. Walichukua simu yake na kompyuta na kukuta picha za kambi.

Kevin anakiri ni kweli alipiga picha hizo lakini anasema hakuwa na nia ya kuzisambaza kwa mtu yeyote.

Kisha Kevin alipelekwa kwenye ofisi ya FSB kwa mahojiano. Kwa sababu alikuwa na umri wa miaka 17 tu, mama yake alikwenda pamoja naye.

Kevin anasema wakili aliyetumwa alimwambia anapaswa kukiri ili kupunguziwa adhabu. Baada ya kutia saini karatasi ya kukiri. Kwa sababu alikuwa bado mdogo, alipelekwa kwenye kituo maalumu, mwendo wa saa mbili kwa gari huko Krasnodar.

"Waliniletea chakula lakini sikuweza kukila. Nilitamani sana kumuona mama yangu."

Miezi michache baadaye, alipofikisha umri wa miaka 18, alihamishiwa kwenye gereza nje kidogo ya Krasnodar ambako alichanganyika na wafungwa wengine.

Kevin anasema alibaki na hofu baada ya kundi la wafungwa kumpiga. "Walinifunga mikono, wakanipiga, na hata kuniwekea sigara. Walinipiga sana kifuani nikashindwa kupumua."

dfc

CHANZO CHA PICHA,FSB

Maelezo ya picha,Maafisa wa FSB wakimuingiza Kevin na mama yake kwenye gari ndogo huko Sochi

Wakati huu wote, mamlaka iliendelea kumchunguza. Mwalimu wake wa darasa alitoa ushahidi dhidi yake, akidai walipokuwa wamekwenda kwenye mashindano ya kitaaluma huko Moscow, Kevin alitaka kwenda kwenye ubalozi wa Ujerumani ili kuwasiliana na maafisa wa ujasusi.

Kevin ananiambia alichotaka ni kupata kitambulisho rasmi cha Ujerumani, kwa sababu alikuwa amefikisha miaka 16.

Mtaalamu wa Wizara ya Ulinzi alichambua picha ambazo Kevin alipiga na kuhitimisha kuwa hazikuwa ni siri ya serikali, lakini zikiwa mikononi mwa mgeni, zingeweza kuidhuru Urusi.

Failil la FSB linajumuisha maelezo ya safari za utotoni kwenda Urusi, moja alipokuwa na umri wa miaka miwili. Kevin anasema pia aligundua kuwa simu yake ilidukuliwa mapema 2021.

Miezi kumi baada ya Kevin kukamatwa, mwishoni mwa Desemba 2023, alipatikana na hatia ya uhaini na kuhukumiwa miaka minne.

Mbali na mama yake, hakuna mtu aliyemfahamu, lakini baada ya vyombo vya habari kuripoti kesi yake, watu wasiojulikana walianza kuwasiliana nae.

"Barua zilinisaidia sana," anasema. "Katika siku yangu ya kuzaliwa, nilipokea kadi 60. Nilikuwa na lengo kumjibu kila mtu." Lakini barua na kadi zilichukuliwa baadaye.

Kubadilishana wafungwa

ED

CHANZO CHA PICHA,FSB

Maelezo ya picha,FSB pia ilionyesha darubini iliyopatikana katika nyumba ya Kevin

Ghafla, alipokuwa akitoka kwenye bafuni Jumanne tarehe 23 Julai, alifikiwa na afisa mkuu wa gereza na kuambiwa ana dakika 20 "kuandika ombi la kuomba msamaha kwa rais, na alifanya hivyo.

Kisha, tarehe 28, ofisa wa gereza alimwambia achukue mswaki, dawa ya meno na viatu. Saa 01:00 asubuhi ya Jumatatu tarehe 29, msafara ulifika kumchukua.

Alisafirishwa hadi Moscow, ambako aliwekwa gerezani hadi Alhamisi 1 Agosti, na kisha kuwekwa kwenye ndege pamoja na wafungwa wengine waliokuwa wakibadilishwa.

Haikuwahi kuelezwa kwamba alikuwa akibadilishwa, anasema, lakini wakati alipokuwa angani kuelekea Uturuki alielewa kinachoendelea.

Muuaji Vadim Krasikov alikuwa miongoni mwa wale waliorejeshwa Urusi, akibadilishwa na yeye.

Huko Ujerumani, baada ya kuchunguzwa hospitalini, hatimaye Kevin aliweza kumsalimia mama yake, ambaye alikuwa amepata viza ya kusafiri kwa ndege kutoka Urusi.

Mama na mwana sasa wanaishi Ujerumani na Kevin anataka kumaliza shule.

"Sina hamu ya kulipiza kisasi, lakini nina hamu kubwa ya kushiriki katika shughuli za upinzani," ananiambia.

Kevin bado ana sare zake za gereza, kwenye begi kwenye kona ya chumba chake.

Comments

Popular posts from this blog

Ukraine yasema inadhibiti makazi 100 ya Warusi

Biden alaani shambulio la Urusi dhidi ya Ukraine

UN yasitisha kutoa msaada Gaza kwasababu ya amri ya kuhama